Wananchi wafurahishwa na elimu ya PBPA katika Maonesho ya Utamaduni

Na Mwandishi wetu, Morogoro

Wananchi waliotembelea banda la Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) katika Maonesho ya Utamaduni mkoani Morogoro, wameeleza kufurahishwa na elimu wanayoipata kuhusu namna mafuta yanavyoagizwa nchini na jukumu la Wakala katika kuratibu mchakato huo.

Wamesema maonesho hayo yamekuwa fursa muhimu ya kupata uelewa kuhusu Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System – BPS) na namna unavyosaidia kuratibu upatikanaji wa mafuta nchini.

Mmoja wa waliotembelea banda hilo, Maria Ngilisho, alisema elimu hiyo imemsaidia kuelewa mchakato wa upatikanaji wa mafuta ambao awali hakuwa na ufahamu wa kutosha kuuhusu.

“Nimefurahi kupata elimu hii kwa sababu tumekuwa tukitumia mafuta kila siku, lakini hatukuwa tunafahamu mchakato unaofanyika hadi mafuta yanapofika nchini. Sasa nimeelewa kuwa kuna taasisi kama PBPA inayoratibu uagizaji wa mafuta kwa pamoja,” alisema.

Naye Michael Maganga alisema mawasiliano ya ana kwa ana na watumishi wa PBPA yamewapa wananchi nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa moja kwa moja kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mafuta.

“Elimu tunayopata hapa ni muhimu sana kwa sababu tunapata nafasi ya kuuliza maswali yanayotuhusu kama watumiaji wa mafuta na tunapata majibu kutoka kwa wataalamu. Ni vizuri PBPA kuendelea kutumia maonesho haya kuwafikia wananchi,” alisema Maganga.

Kwa mujibu wa PBPA, miongoni mwa majukumu ya Wakala ni kukusanya mahitaji ya mafuta kutoka kwa kampuni za uuzaji wa mafuta, kuendesha zabuni za kimataifa za ununuzi wa mafuta kwa wingi, pamoja na kuratibu upokeaji na uwasilishaji wa bidhaa hizo nchini.

Mfumo huo unalenga kuwezesha uagizaji wa mafuta kwa pamoja, hatua inayosaidia kuratibu mahitaji ya soko na kuhakikisha bidhaa hiyo muhimu inapatikana kwa uhakika nchini.

Ushiriki wa PBPA katika maonesho mbalimbali ni sehemu ya juhudi za Wakala za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu yake na nafasi yake katika sekta ya mafuta.

Kupitia maonesho hayo, wananchi pia hupata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu kuhusu mchakato wa uagizaji wa mafuta na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hiyo unaendelea kuwa wa uhakika nchini.