Tume ya utumishi wa umma yaipongeza wizara ya nishati kwa kuzingatia sheria

DODOMA.

Wizara ya Nishati imepongezwa kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yake.

Pongezi hizo zimetolewa Septemba 14, 2026 na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Omari Kitenge, wakati wa kikao kati ya Tume hiyo na Menejimenti ya Wizara ya Nishati kilichofanyika Mtumba, Dodoma.

Kikao hicho kililenga kuhitimisha zoezi la Ukaguzi wa Uzingatiaji wa Sheria katika Utumishi wa Umma (Exit Meeting) lililofanywa na Tume katika Wizara hiyo.

Aidha, Wizara imepongezwa kwa kufanyia kazi hoja zote zilizoainishwa na Tume wakati wa ukaguzi wa mwaka 2023, jambo lililoelezwa kuwa ni ishara ya utayari wa kuendelea kuimarisha uzingatiaji wa miongozo na taratibu za Utumishi wa Umma.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Makatibu Wakuu, Petro Lyatuu, ameishukuru Tume kwa kufanya ukaguzi huo, akisema umesaidia Wizara kubaini maeneo yenye changamoto na kuyafanyia kazi ili kuboresha utekelezaji wa majukumu na utoaji wa huduma kwa wananchi.