Wakulima washauri mbegu asili ziuzwe madukani


WAKULIMA  wanaotumia mbinu za kilimo ikolojia wameishauri Serikali kuhakikisha maduka ya pembejeo yanauza mbegu, mbolea na viuatilifu vya asili ili kurahisisha upatikanaji wake.

Ushauri huo umetolewa jana Arusha wakati wa uzinduzi wa miradi mitatu ya IDP, ikiwemo Kilimo Endelevu Arusha+ II, ECO-FOOD II na SAFI Project, inayolenga kuimarisha kilimo endelevu na mifumo ya chakula.

Mkulima kutoka Karatu, Bakari Sumawe, amesema wakulima wengi wamehamasika kutumia mbinu hizo, lakini upatikanaji wa mbegu za asili bado ni changamoto.

Mkulima wa mbogamboga kutoka Oldonyowas, Flora Mollel, amesema miradi hiyo imeleta mabadiliko kwa wakulima, akitaka Serikali kushirikiana na wadau kuwafikia wakulima wengi zaidi.

Wakulima na wazalishaji wa pembejeo pia wametaja ukosefu wa masoko na zana za uzalishaji kuwa changamoto, huku Mkurugenzi wa IDP, Ayesiga Buberwa, akisema ECO-FOOD II inalenga kuongeza thamani na masoko ya bidhaa za kilimo ikolojia.

Amesema SAFI Project inalenga kuboresha upatikanaji wa pembejeo hai, mashine na vifaa vidogo vya kilimo, hususan kwa wanawake. Uzinduzi wa miradi hiyo umefanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa Arusha DC, Suleiman Msumi.