ZANZIBAR:
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameiagiza Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kuanza mchakato wa kuanzisha Kitengo Maalum cha Kilimo Hai kwa ajili ya kuratibu na kusimamia shughuli za kilimo hicho visiwani.
Agizo hilo amelitoa Septemba 23 katika Viwanja vya Dole Nane Nane wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Kilimo Hai Zanzibar (Zanzibar Organic Festival), lenye kaulimbiu “Fikiri Kiulimwengu, Kula Kiasili”.
Rais Mwinyi amesema Serikali imezindua Mkakati wa Kilimo Hai Zanzibar na sasa inapaswa kuhakikisha utekelezaji wake unaonekana katika bajeti, huduma za ugani, pembejeo, tafiti na mnyororo wa thamani.
Aidha, ameitaka Wizara kufanya tathmini ya uwezekano wa kuingiza pembejeo za kilimo hai katika mpango wa ruzuku ili kupunguza gharama kwa wakulima.
Amesema Serikali itaendelea kudhibiti matumizi yasiyodhibitiwa ya pembejeo za kemikali na kutoa elimu kwa wakulima, huku akisisitiza umuhimu wa uzalishaji wa chakula salama na uhifadhi wa rutuba ya udongo na maji.
Dk. Mwinyi pia amesema ukuaji wa utalii Zanzibar unatoa fursa kwa wakulima, akitoa wito kwa hoteli na migahawa kuongeza ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima wa Zanzibar kupitia mfumo wa “Shambani Hadi Mezani”.
Awali, Mwenyekiti wa tamasha hilo, Iqram Soraga, alimuomba Rais Mwinyi kuanzisha kitengo hicho pamoja na kutoa ruzuku kwa pembejeo za kilimo hai.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Island of Peace (IDP), Richard Libent, amesema wamepokea kwa furaha hatua hiyo na kuomba mfumo wa tamasha hilo kuenezwa pia Tanzania Bara ili kukuza kilimo hai na ikolojia nchini.



