DAR ES SALAAM:
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza awamu ya kwanza ya upangaji wa mikopo na ruzuku kwa wanafunzi waliodahiliwa katika vyuo mbalimbali nchini kwa mwaka wa masomo 2026/2027, ambapo jumla ya Sh. bilioni 535.7 zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi 165,775.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 10, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema fedha hizo zitanufaisha wanafunzi wa ngazi ya Stashahada, shahada ya awali pamoja na wanafunzi wanaoendelea na masomo.
Katika mchanganuo wa awamu hiyo ya kwanza, HESLB imewapangia mikopo wanafunzi 74,769 wa shahada ya awali, yenye thamani ya Sh. bilioni 246.8.
Kwa upande wa wanafunzi wa Stashahada, jumla ya wanafunzi 8,538 wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 22.9.
Aidha, wanafunzi wapya 873 wamepangiwa ruzuku kupitia mpango wa Samia Scholarship, yenye thamani ya Sh. bilioni 4.5.
Kwa wanafunzi wanaoendelea Bodi imetenga Sh. bilioni 252.4 kwa ajili ya wanafunzi 79,115 wa shahada ya awali, Sh. bilioni 3.8 kwa wanafunzi 1,554 wa Stashahada, pamoja na Sh. bilioni 5.1 kwa wanafunzi 926 wanaonufaika na Samia Scholarship.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Dkt. Kiwia amesema bajeti ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2026/2027 imeongezeka kutoka Sh. bilioni 916.7 mwaka uliopita hadi Sh. trilioni 1.06 mwaka huu.
Amesema ongezeko hilo la bajeti linalenga kupanua wigo wa upatikanaji wa mikopo na ruzuku ili kufikia wanafunzi wapatao 329,000 kwa ujumla katika mwaka huu wa masomo.
Aidha, idadi ya wanafunzi wapya wanaonufaika na mikopo imeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita, hatua inayolenga kuwasaidia wanafunzi wengi zaidi kupata fursa ya kuendelea na elimu ya juu.
Katika hatua nyingine, HESLB imewataka wanafunzi wote walioomba mikopo kuingia katika akaunti zao za mfumo wa SIPA (Student Individual Permanent Account) ili kukamilisha taratibu zinazohitajika kwa ajili ya kupokea fedha zao.
Wanafunzi hao wanatakiwa kuhakikisha wameweka taarifa sahihi za akaunti zao za benki na namba za simu ili kurahisisha upelekaji wa fedha na kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa malipo.
Kwa wanafunzi wenye sifa za kupata mikopo ambao majina yao hayajaonekana katika awamu ya kwanza, HESLB imewataka kutokuwa na wasiwasi na badala yake wametakiwa kuendelea kufuatilia matangazo kupitia njia rasmi za Bodi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mchakato wa uchambuzi wa maombi unaendelea kulingana na taarifa za udahili zinazopokelewa kutoka vyuoni, huku awamu nyingine za upangaji mikopo zikitarajiwa kutangazwa kabla ya mwisho wa Oktoba 2026.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanapata fursa ya kuzingatiwa katika awamu zinazofuata za upangaji wa mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
