Maonesho hayo yanayojulikana kama ZIFF Goes Mainland Film Festival 2026 yatafanyika Dar es Salaam, Bagamoyo, Mwanza, Iringa na Dodoma, huku wananchi wakipata fursa ya kutazama filamu bure na kushiriki mijadala kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii na kiteknolojia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Joseph Mwale, amesema ushirikiano kati ya taasisi hiyo na Umoja wa Ulaya umedumu kwa miaka mingi, huku programu ya kupeleka filamu Tanzania Bara ikifikia toleo la tano mwaka huu.
Amesema filamu zitakazooneshwa zitatoka Tanzania na nchi za Ulaya, zikijadili masuala ya akili unde (AI), mabadiliko ya tabianchi, teknolojia na nafasi ya binadamu katika dunia inayobadilika.
Ameeleza kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inalenga kuunganisha ulimwengu wa kidijitali na maisha ya binadamu, kwa kuonesha uhusiano uliopo kati ya teknolojia, mazingira na maisha ya kila siku.
Amesema tasnia ya filamu pia inaweza kuwa chanzo cha ajira kwa vijana kupitia utengenezaji wa filamu, ufundi na ujasiriamali wa kidijitali.
Mbali na maonesho hayo, programu hiyo itatoa fursa kwa wanafunzi kufahamu zaidi kuhusu Erasmus+, programu ya Umoja wa Ulaya inayosaidia elimu na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma, ikiwemo fursa za masomo barani Ulaya.
Filamu itakayofungua maonesho hayo kesho katika kituo cha Alliance Française jijini Dar es Salaam ni A Land Apart, filamu ya kusisimua ya kisayansi kutoka Nigeria iliyoshinda tuzo katika ZIFF 2026.
Baada ya Dar es Salaam, maonesho yataendelea katika vituo vya elimu na utamaduni, ikiwemo TASUBA Bagamoyo, Chuo Kikuu cha St. Augustine Mwanza, Chuo Kikuu cha Ruaha Iringa na Chuo Kikuu cha Dodoma.

