Serikali imeendelea kufungua fursa kwa wachimbaji wadogo nchini baada ya kutenga eneo la Nyakafulu wilayani Mbogwe mkoani Geita na kutoa leseni 108 za uchimbaji.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ajira, kurasimisha shughuli za uchimbaji mdogo na kuwapa wananchi ushiriki kwenye uchumi wa madini.

Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa amesema hatua hiyo imekuja baada ya baadhi ya leseni kufutwa kutokana na kutoendelezwa ipasavyo.

“Serikali kupitia Tume ya Madini inaendelea kufanya tathmini ya leseni ambazo hazijaendelezwa ili baadhi ya maeneo hayo yatengwe kwa wachimbaji wadogo,” amesema.

Kwa mujibu wa Serikali, leseni 63 za utafiti bado zinafanyiwa tathmini ya kisheria kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.

Serikali pia imesema itaendelea kutumia taarifa za jiosayansi kubaini maeneo yenye madini yanayoweza kunufaisha wachimbaji wadogo, huku STAMICO ikiendelea kufanya tafiti za kina kwenye baadhi ya maeneo.

Serikali imesema ipo kwenye hatua za mwisho za uhakiki wa madai ya waliokuwa wafanyakazi wa Mgodi wa Kiwira kabla ya kuanza kulipa deni la Tshs. Bilioni 1.52.

Akijibu swali la Mbunge wa Kyela, Bungeni Dodoma, Mhe. Kiruswa amesema madai hayo yalitokana na malalamiko ya wafanyakazi kuhusu mafao yao baada ya ubinafsishaji wa mgodi huo.

Kwa mujibu wa uhakiki uliofanyika, madai halali ya wafanyakazi 893 yalifikia TZS 1.024 bilioni, tofauti na madai ya awali yaliyokuwa yanazidi Tshs. 47 bilioni.

Amesema Serikali tayari imeingiza deni hilo kwenye orodha rasmi ya madeni ya Serikali huku uhakiki wa mwisho ukiendelea kabla ya malipo kuanza.

Soma