Shinyanga kupata kivutio kipya cha utalii kupitia Lubaga Forest

Na Mwandishi wetu, Shinyanga 

Wapenzi wa utalii wa asili, matembezi ya msituni na mandhari ya kuvutia wanatarajia kupata kivutio kipya baada ya Kituo cha Utalii Ikolojia cha Lubaga Forest kufunguliwa rasmi Juni 27, 2026 mkoani Shinyanga.

Kituo hicho, kilichoendelezwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilaya ya shinyanga, kinatarajiwa kuufungua Msitu wa Lubaga kwa wageni wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuhamasisha utalii wa asili, uhifadhi wa mazingira na kuwapa wananchi nafasi ya kujifunza kuhusu umuhimu wa misitu.

Kupitia kituo hicho, wageni watapata fursa ya kufanya matembezi ya msituni, kuendesha baiskeli, kupiga picha, camping, picnic, katika maeneo yenye mandhari ya kuvutia pamoja na kufurahia mazingira ya utulivu na mapumziko katikati ya asili.

Kwa mujibu wa TFS wilaya ya Shinyanga, mradi huo ni sehemu ya juhudi za kuanzisha bidhaa mpya za utalii nchini na kuonyesha kuwa misitu inaweza kuwa chanzo cha burudani, elimu na fursa za kiuchumi kwa jamii zinazozunguka maeneo hayo.

"Lubaga Forest ni zaidi ya msitu. Ni mahali ambapo watu wataweza kukutana na asili, kujifunza kuhusu bioanuwai na kutambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho," imesema TFS Wilaya ya Shinyanga.

Mbali na kuvutia watalii, kituo hicho kinatarajiwa kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wakazi wa Shinyanga kupitia biashara zinazohusiana na utalii, huduma za wageni na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.

Uzinduzi wa Lubaga Forest Ecotourism Centre unakuja wakati Tanzania ikiendelea kupanua wigo wa sekta ya utalii kwa kuendeleza vivutio vipya nje ya hifadhi za wanyamapori na fukwe, huku utalii wa ikolojia ukionekana kuwa moja ya maeneo yenye ukuaji mkubwa duniani.

Kuanzia Juni 27, wageni wa kwanza watapata nafasi ya kujionea kile ambacho TFS inakiita “mahali ambapo mioyo hukutana na asili” – eneo linalounganisha uhifadhi, burudani, elimu na kumbukumbu zisizosahaulika.