Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania yasisitiza matumizi ya maktaba mtandao


Na Mwandishi wetu 

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) imewahimiza wananchi kutumia huduma ya maktaba mtandao ya kitaifa, ili kurahisisha upatikanaji wa vitabu na taarifa mbalimbali kutoka katika maktaba za umma nchini.

Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma, Mkutubi wa Maktaba ya Mkoa wa Dodoma, Edward Fungo, alisema bodi imeanzisha mfumo wa maktaba mtandao unaowawezesha wananchi kujisajili na kupata huduma za maktaba kwa njia ya kidijitali.

“Hatua ya kwanza tumewawezesha wananchi kujisajili na kuona vitabu vilivyopo kwenye maktaba zetu zote. Hii ni sehemu ya jitihada za serikali za kuhamasisha taasisi kutumia mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma,” alisema Fungo.

Kwa mujibu wa TLSB, wananchi wanaweza kuingia katika mfumo huo kupitia anuani ya idlibtaifa.tlsb.go.tz/login, kujisajili na kuanza kutafuta vitabu vinavyopatikana katika maktaba zote 43 zilizounganishwa kwenye mtandao wa maktaba ya taifa.

TLSB imeanza kusogeza huduma za maktaba karibu na wananchi kupitia mpango wa maktaba jamii, ambapo vituo vya kwanza vimefunguliwa MACOBIKA, wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, na Bustani mkoani Kilimanjaro.

Huduma hizo zinalenga kuchangia utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya taifa kwa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania kupitia Kitengo cha Maktaba ya Taifa kinatoa huduma za usajili wa vitabu na majarida, ikiwemo utoaji wa namba za utambulisho za vitabu (ISBN) na majarida (ISSN).

Bodi pia inawataka waandishi, wachapishaji binafsi na taasisi mbalimbali kutumia huduma hiyo ili kuhifadhi machapisho yao kama sehemu ya kumbukumbu za taifa na kurahisisha upatikanaji wa nyaraka kwa watafiti wa sasa na wa baadaye.

Kutokana na takwimu za elimu, umuhimu wa kujenga utamaduni wa kusoma kuanzia ngazi ya watoto wa shule za msingi, umekuwa ni hatua ya msingi katika kujenga taifa lenye utamaduni wa kujisomea na kujiendeleza.

“Tunawahimiza Watanzania kutumia maktaba zetu zote 45, zikiwemo maktaba jamii mbili mpya, ili kupata maarifa na taarifa zinazowasaidia katika maendeleo yao,” alisema.