Na Mwandishi wetu

Dodoma. Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imewataka wakulima nchini kuwa makini na matumizi ya taarifa zao binafsi wanapotumia mifumo ya kidigitali katika uzalishaji, masoko na shughuli nyingine za kilimo.

PDPC imesema matumizi ya teknolojia katika kilimo yanaendelea kukua, jambo linalofanya taarifa za wakulima kukusanywa, kuhifadhiwa na kubadilishana kupitia mifumo mbalimbali ya kidigitali.

Akizungumza katika Maonyesho ya Nane Nane, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia ailisema usalama wa taarifa binafsi ni muhimu katika kujenga uaminifu kati ya wakulima, wanunuzi, taasisi za fedha, kampuni za teknolojia na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa kilimo.

"Unapotambua masoko, maana yake pia itahusisha mifumo ya kidigitali na kubadilishana taarifa mbalimbali, ambazo baadhi yake ni taarifa za faragha," alisema Dkt. Mkilia.

PDPC imeeleza kuwa wakulima wanapaswa kufahamu haki zao kuhusu taarifa zao binafsi na namna taarifa hizo zinavyotumiwa na taasisi au mifumo wanayoshirikiana nayo.

Kauli mbiu ya Nane Nane ya mwaka huu, "Tambua soko, ongeza tija katika utekelezaji wa Dira ya 2050," inaendana na umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kutafuta masoko na kuongeza tija.

Tume inaendelea kusisitiza kwa kuwataka wakulima kuhakikisha taarifa zao hazitolewi au kutumiwa bila kufuata taratibu zinazolinda faragha na usalama wa mhusika.

Elimu hiyo ni muhimu zaidi wakati Tanzania inaendelea kuelekea kwenye uchumi wa kidigitali, ambapo teknolojia inatarajiwa kuchukua nafasi kubwa katika sekta ya kilimo, ikiwemo uzalishaji, masoko na huduma za kifedha.

"Msisitizo wetu ni kuhakikisha taarifa hizi zinalindwa na zinatumika ipasavyo kwa kuzingatia faragha ya watu wote wanaohusika katika mnyororo mzima wa shughuli za kilimo," alisisitiza Mkurugenzi.

Kwa upande mwingine, Tume imewataka wakulima kutumia fursa za teknolojia kuongeza tija na kufikia masoko, huku wakihakikisha wanachukua hatua za msingi kulinda taarifa zao.

Kwa mujibu wa Tume, ulinzi mzuri wa taarifa binafsi unasaidia kujenga uaminifu na kuwawezesha wakulima kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali bila kuhatarisha faragha na usalama wa taarifa zao.