Na Mwandishi wetu
Dodoma – Kiongozi mstaafu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Deogratius Aloyce Maneno, amesema uwekezaji katika mfumo wa vipimo sahihi ni muhimu katika kujenga uchumi imara, kulinda wafanyabiashara na kuhakikisha soko linakuwa la haki kwa wote.
Maneno, ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa WMA, alisema hayo jana, Agosti 8, 2026, alipotembelea banda la Wakala huo katika Maonesho ya 33 ya Wakulima (Nanenane) yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Dodoma.
Alisema amefurahishwa na maendeleo aliyoyaona WMA, akibainisha kuwa taasisi hiyo imepiga hatua katika matumizi ya vifaa na utoaji wa elimu kuhusu vipimo ikilinganishwa na kipindi alichokuwa akihudumu.
“Nimefurahishwa sana kuona WMA imepiga hatua kubwa. Tulipoanza tulikuwa na changamoto za vifaa na uelewa, lakini leo naona vijana wanasimama wenyewe kutoa elimu. Hii ndiyo tija ya uwekezaji,” alisema.
Hata hivyo, Maneno alisema elimu kuhusu vipimo haipaswi kuishia kwa wafanyabiashara wakubwa, bali inapaswa kuwafikia pia wafanyabiashara wadogo ambao kwa kiasi kikubwa wanahusika moja kwa moja na matumizi ya vipimo katika biashara za kila siku.
“Huu ni wakati wa kushuka ngazi hadi kwa mama lishe na wauza bidhaa sokoni, maana ndio wanaoumia zaidi na vipimo visivyo rasmi,” alisema.
Alishauri wafanyabiashara kutumia teknolojia katika shughuli zao, ikiwemo mizani ya kidijitali na mifumo ya utoaji wa risiti, akisema hatua hiyo inaweza kusaidia kuweka kumbukumbu sahihi za miamala na kupunguza mianya ya ubadhirifu.
“Dunia imebadilika. Tumieni mizani ya kidijitali zaidi na mifumo ya kutoa risiti. Hii itasaidia kuwa na rekodi na kupunguza ubadhirifu katika biashara,” alisema.
Maneno pia aliwataka watendaji wa WMA kutumia mamlaka waliyopewa na sheria kuhakikisha wafanyabiashara wanaokiuka taratibu za vipimo wanachukuliwa hatua.
“WMA ina mamlaka. Itumieni. Mkikamata na kutoa faini kwa wale wanaokiuka, wengine watafuata sheria. Soko la haki linahitaji nidhamu,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa WMA, Veronica Simba, alisema taasisi hiyo inathamini mchango wa viongozi na watendaji wastaafu walioweka misingi ya utendaji wa Wakala.
Alisema uzoefu wa viongozi hao unaendelea kuwa muhimu katika kuboresha huduma za WMA na kuhakikisha wananchi wanapata vipimo sahihi katika shughuli zao za kiuchumi.
Wastaafu wengine waliotembelea banda la WMA katika maonesho hayo ni Evarist Masengo, aliyewahi kuwa Meneja wa WMA wa Mkoa, na Joseph Maliti, aliyewahi kuwa Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi.
Walisema wamefurahishwa na maendeleo ya WMA na kupongeza uongozi pamoja na watumishi kwa kuendeleza huduma za vipimo nchini.
