SwissAid: Wakulima 16,000 kunufaika na awamu ya pili ya mradi wa kilimo ikolojia

Na Mwandishi wetu

Lindi. Shirika la SwissAid Tanzania limesema linaendelea kuimarisha kilimo ikolojia nchini kupitia mradi wa miaka 10 wenye thamani ya zaidi ya Tsh bilioni 10, unaolenga kuongeza uzalishaji wa mazao, kuhifadhi mbegu za asili na kuboresha lishe kwa wananchi.

Akizungumza katika Maonesho ya Tano ya Vyakula na Mbegu za Asili yaliyofanyika mkoani Lindi, Mkurugenzi Mkazi wa SwissAid Tanzania, Betty Malaki, alisema awamu ya pili ya mradi huo inalenga kuwafikia wakulima 16,000, mara mbili ya idadi ya walionufaika katika awamu ya kwanza.

Alisema asilimia 70 ya wanufaika wa awamu hiyo watakuwa wanawake, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uzalishaji wa chakula, uongozi na shughuli za kiuchumi.

"Ushiriki wenu unaonesha dhamira ya pamoja ya kuendeleza kilimo endelevu, kuboresha mifumo ya chakula na kuinua maisha ya wakulima nchini," alisema Malaki.

Alieleza kuwa maonesho hayo, yanayoadhimishwa kila mwaka Agosti 6 katika Kanda ya Kusini, yanalenga kuhamasisha matumizi ya vyakula vya asili vyenye lishe na kuhifadhi mbegu za asili kwa ajili ya usalama wa chakula na afya ya jamii.

Malaki alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa kuridhia tarehe hiyo kuwa siku maalumu ya maonesho ya vyakula na mbegu za asili, akisema hatua hiyo imeongeza hamasa ya wadau na wakulima kushiriki katika uhifadhi wa rasilimali za kilimo.

Alisema mradi wa "Crops for Healthier Diets (Crops4HD)" ulianza mwaka 2019, ambapo awamu ya kwanza iliyokamilika mwaka 2025 iliwafikia zaidi ya wakulima 8,000 waliopatiwa mafunzo ya kilimo ikolojia, uhifadhi wa mbegu za asili na kuongeza thamani ya mazao.

Kwa mujibu wake, awamu ya pili ilianza Julai 2025 na itaendelea hadi Juni 2029, huku utekelezaji wa mradi mzima ukitarajiwa kukamilika mwaka 2030.

Aidha, alisema mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Uswisi kupitia Swiss Agency for Development and Cooperation (SDC), Tume ya Ulaya kupitia Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) pamoja na LDS Charitable Foundation, kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali zikiwemo SAT, RECODA, TARI, TFCG na washirika wengine.

Malaki pia aliishukuru Serikali ya Tanzania, Wizara ya Kilimo, mikoa ya Lindi na Mtwara, pamoja na taasisi za utafiti na elimu kama TARI na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa ushirikiano wao katika kuendeleza tafiti na teknolojia zinazochochea maendeleo ya kilimo ikolojia nchini.