Na Atley Kuni, WAF-Mbeya
Mkuu wa Mkoa Mteule wa Mbeya, Mhe. Jumanne Sagini, amewataka waganga, wauzaji na wazalishaji wa dawa za Tiba Asili nchini kuhakikisha vituo vyao vinasajiliwa kwa mujibu wa sheria, akisisitiza kuwa maendeleo ya sekta hiyo yanapaswa kuambatana na weledi, usalama, ubora, uadilifu na ushahidi wa kisayansi.
Agizo hilo limetolewa leo, Agosti 31, 2026, na Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mhe. Jafar Haniu, kwa niaba ya Mhe. Sagini, wakati wa kilele cha Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika kilichofanyika katika Viwanja vya Uhindini jijini Mbeya. Amesema Serikali imeendelea kurahisisha usajili wa watoa huduma na kwamba tangu kuanza kwa utaratibu wa kusogeza huduma za utambuzi na usajili karibu na wananchi mwaka 2007, zaidi ya wataalamu 70,000 wa Tiba Asili wamesajiliwa.
Amesema hatua hiyo imeenda sambamba na usajili wa dawa, ambapo hadi sasa dawa 196 za Tiba Asili zimesajiliwa baada ya kufanyiwa tathmini na vipimo vya maabara kwa mujibu wa miongozo iliyowekwa. Aidha, Serikali imefikisha huduma za Tiba Asili katika hospitali 14 za rufaa za mikoa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, ambapo tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo mwaka 2023, zaidi ya wagonjwa 2,300 wamehudumiwa kupitia mfumo huo.
Akizungumzia uzalishaji wa malighafi, Mhe. Sagini amesema kila halmashauri ina jukumu la kutenga eneo lenye ukubwa wa ekari 50 au zaidi kwa ajili ya kilimo, uhifadhi na uvunaji endelevu wa mimea dawa. Amesema hatua hiyo inalenga kujenga mnyororo wa thamani unaowaunganisha wakulima, watafiti na viwanda, huku ukifungua fursa za ajira, uwekezaji na uzalishaji wa dawa zinazoweza kushindana katika masoko ya kimataifa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Sagini ameonya kuhusu ongezeko la matangazo ya dawa na huduma za Tiba Asili kwenye vyombo vya habari, mabango na mitandao ya kijamii, akisema matangazo yasiyozingatia sheria yanaweza kupotosha wananchi na kuhatarisha afya zao. Amesema Tiba Asili haipaswi kuangaliwa kama suala la afya pekee, bali ni sekta mtambuka yenye uwezo wa kuchangia katika kilimo, viwanda, ajira, biashara, utalii na ukuaji wa uchumi.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Sagini amezitaka taasisi za utafiti, vyuo vikuu, sekta binafsi na wadau wengine kuimarisha tafiti na ubunifu ili maarifa ya Tiba Asili yageuzwe kuwa bidhaa zenye ushahidi wa kisayansi, ubora na thamani ya kibiashara. Pia amewataka watoa huduma ambao bado hawajasajili vituo vyao kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria, akisisitiza dhamira ya Serikali ya kuona Tiba Asili ya Tanzania inavuka mipaka na bidhaa zake kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.








