Bodi ya ushauri TARURA yakagua barabara za kuingia uwanja wa AFCON Arusha

ARUSHA.

Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara za kuingia katika Uwanja wa AFCON Arusha, huku utekelezaji wa mradi huo ukifikia zaidi ya asilimia 60.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Florian Kabaka, amesema ameridhishwa na maendeleo ya mradi huo na kusisitiza kasi ya utekelezaji wa kazi zinazoweza kukamilishwa kabla ya kuanza kwa mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu.

Mhandisi Kabaka amesema ziara hiyo imelenga kujionea maendeleo ya miradi mbalimbali, kukagua utekelezaji wa mikataba na kutoa ushauri kwa wahusika ili kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Amesema kwa ujumla miradi inayotekelezwa inaendelea vizuri, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia ratiba na kuchukua hatua mapema dhidi ya changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua. Pia amemtaka mkandarasi kuzingatia utabiri wa hali ya hewa na kuzipa kipaumbele kazi zinazoweza kufanyika kabla ya mvua.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, amesema ziara hiyo imehusisha ukaguzi wa barabara zinazounganisha maeneo mbalimbali ya Uwanja wa AFCON, huku lengo likiwa ni kuhakikisha mradi unakamilika ifikapo Mei 2027.

Mhandisi Seff amemtaka Mhandisi Mshauri, M/s Afrisa Consulting LTD, kusimamia kwa karibu utekelezaji wa kazi, huku akimtaka mkandarasi, M/s China Railway Construction Engineering Group, kufanya tathmini upya ya utayari wa mradi kukabiliana na mvua za El Niño na kuwasilisha taarifa hiyo ili hatua stahiki zichukuliwe.