DAR ES SALAAM
Michezo imeendelea kuwa sehemu muhimu ya kujenga afya, mshikamano na mahusiano mazuri kazini, huku taasisi mbalimbali zikihamasishwa kuendeleza shughuli zinazowakutanisha watumishi nje ya majukumu yao ya kawaida.
Kwa kuzingatia hilo, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imeandaa Bonanza la Michezo katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), likilenga kuimarisha afya, umoja na mshikamano wa wafanyakazi.
Bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, riadha, kuvuta kamba, kimbiza kuku, mbio za magunia pamoja na michezo ya burudani.
Akizungumza katika bonanza hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Athumani Mombokaleo, amesema michezo hiyo ni sehemu ya kujenga afya na mahusiano miongoni mwa wafanyakazi, lakini pia inatoa nafasi ya kutambua mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya usafiri wa anga.
Amesema moja ya mafanikio hayo ni kutambuliwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kuwa miongoni mwa viwanja bora vya ndege barani Afrika, akieleza kuwa ni heshima na fahari kwa Tanzania.
Mombokaleo amesema mafanikio hayo yamechangiwa na wadau mbalimbali na yanapaswa kutambuliwa kwa pamoja, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha huduma za viwanja vya ndege kwa kuwa ni miongoni mwa milango muhimu ya kuingia na kutoka nchini.
Amesema ubora wa huduma katika viwanja vya ndege una nafasi katika kujenga imani kwa watalii, wawekezaji na wafanyabiashara wanaoingia nchini.
Katika hatua nyingine, Mombokaleo ametangaza mpango wa TAA kuanzisha Airport Marathon, itakayofanyika mara moja au mbili kwa mwaka kwa lengo la kukuza michezo, afya na taswira nzuri ya viwanja vya ndege nchini.
Aidha, amezitaka taasisi za serikali na binafsi kushirikiana katika kuandaa mabonanza ya michezo ya pamoja ili kuimarisha ushirikiano na mshikamano miongoni mwa watumishi.
