Na OWM–TAMISEMI,
Kilwa – Lindi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amezitaka wilaya na halmashauri zote nchini kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba 2026 hadi Februari 2027.
Prof. Shemdoe ametoa agizo hilo Septemba 13, 2026, akiwa Somanga, Wilaya ya Kilwa, wakati akiendelea na ziara ya kikazi mkoani Lindi, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuzibua mitaro na mifereji ya maji pamoja na kuhakikisha miundombinu ya kupitisha maji inakuwa katika hali nzuri.
Amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Mameneja wa TARURA kushirikiana na wananchi na taasisi nyingine kuchukua hatua za mapema ili kuzuia maji kujaa na kuvamia makazi ya wananchi.
“Nimuelekeze Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kushirikiana na wananchi kuzibua mifereji ya maji iliyoziba ili kipindi cha mvua za El Niño maji yasipate nafasi ya kuchepuka na kuvamia makazi ya wananchi na kuleta madhara. Mkuu wa Wilaya ya Kilwa simamia jambo hili,” amesema Prof. Shemdoe.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, Septemba 11, 2026, kwa Wizara, Mamlaka na Taasisi zinazohusika kuchukua hatua za mapema kupunguza athari za mvua hizo, pamoja na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu kuboresha usafi wa mazingira katika miji na majiji.
Katika hatua nyingine, Prof. Shemdoe amemuelekeza Meneja wa TARURA kufanya tathmini ya gharama za ukarabati wa barabara ya Kinjumbi yenye urefu wa kilomita 30 kwa kiwango cha changarawe, baada ya wananchi kuomba ijengwe kwa kiwango cha lami.
Amesema ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami unaweza kuchukua muda mrefu, hivyo tathmini hiyo itasaidia kuangalia uwezekano wa kutumia fedha za matengenezo kuikarabati na kuiwezesha kupitika muda wote.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Somanga, mkazi wa Kata ya Somanga, Hashimu Omary Changadua, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika eneo hilo, ikiwemo ujenzi wa shule mbili za sekondari, soko la kimkakati na kituo cha afya.
Baada ya kuzungumza na wananchi, Prof. Shemdoe aliendelea na ziara yake kwa kukagua ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao linalojengwa na Halmashauri ya Kilwa pamoja na soko la wajasiriamali wadogo katika kijiji cha Njianne, Kata ya Tingi.






