Mameneja TARURA watakiwa kukagua madaraja na makalavati kabla ya mvua


Arusha.

Mameneja wa mikoa na wilaya wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wametakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ya barabara, ikiwemo madaraja na makalavati, ili kuhakikisha usalama na upitishaji wa huduma wakati wa mvua za El Niño.

Akizungumza na Menejimenti na wafanyakazi wa TARURA Mkoa wa Arusha, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, amesema ukaguzi unapaswa kufanyika kuanzia ngazi za chini na maeneo hatarishi kuripotiwa Makao Makuu kwa hatua zaidi.

Amesema barabara zinazotumiwa na wananchi katika shughuli zao za kila siku zinapaswa kuwa salama na kupitika kabla, wakati na baada ya mvua, huku akisisitiza pia usalama wa watumishi na wataalamu wanaofanya ukaguzi katika kipindi hicho.

Aidha, Mhandisi Seff amewataka mameneja kuwasilisha mipango ya utayari wa kukabiliana na mvua hizo, ikiwemo kubainisha wakandarasi walio karibu na maeneo yao ili miundombinu itakapoharibika, hatua za kurejesha huduma zichukuliwe kwa haraka.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha na Mwenyekiti wa Mameneja wa Mikoa wa TARURA, Mhandisi Nicholous Francis, amesema wameanza kutekeleza maelekezo hayo kwa kushirikiana na mameneja wa wilaya, ikiwemo kubaini maeneo yanayoweza kukumbwa na mafuriko na kuandaa timu za kukabiliana na changamoto.

Amesema maeneo yatakayobainika kuwa hatarishi yanaweza kufungwa kwa muda na wananchi kupewa njia mbadala, huku akiwataka wananchi kutovuka barabara zenye maji mengi kwa kuwa kina cha maji hakiwezi kutambulika kwa kuangalia kwa macho.

Mhandisi Francis pia amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto hawaendi kucheza kwenye makorongo au maeneo mengine hatarishi wakati wa mvua.

Aidha, amewataka wamiliki wa shule zinazotumia magari kuwachukua wanafunzi kurekebisha ratiba za usafiri, hasa nyakati za alfajiri na usiku, ili kupunguza uwezekano wa kutokea kwa ajali zinazoweza kuzuilika.