Bangkok, Thailand
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, leo ameshiriki katika ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Kimataifa wa Nishati wa Gastech 2026, unaofanyika Bangkok, Thailand, ukiwakutanisha viongozi wa Serikali, wataalamu, wawekezaji na wadau mbalimbali wa sekta ya nishati kutoka zaidi ya nchi 150 duniani.
Gastech 2026 inafanyika katika kipindi ambacho mahitaji ya nishati duniani yanaendelea kuongezeka kutokana na ongezeko la watu na upanuzi wa viwanda, huku changamoto za kijiografia na kisiasa, kuvurugika kwa mifumo ya usambazaji na mabadiliko ya masoko zikiendelea kuathiri usalama wa nishati duniani.
Katika mkutano huo, gesi asilia, LNG, umeme, teknolojia za kupunguza hewa ukaa na Akili Bandia (AI) vinajadiliwa kama miongoni mwa nyenzo muhimu katika kuimarisha usalama wa nishati, unyumbufu wa mifumo ya nishati na ustahimilivu wa viwanda.
Gastech 2026 inatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya wataalamu 50,000 wa sekta ya nishati kutoka zaidi ya nchi 150 na kufunguliwa Rasmi na Waziri Mkuu wa Thailand Mhe. Anutin Charnvirakul.






