Bunge lapitisha marekebisho ya sheria saba za ardhi, serikali za mitaa na wanyamapori

Na Mwandishi wetu

Dodoma. Bunge limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2, wa mwaka 2026.

Sheria hizo zinahusu matumizi ya ardhi, serikali za mitaa, usalama wa taifa, umiliki wa mali na maliasili, uthamini wa mali pamoja na uhifadhi wa wanyamapori.

Akiwasilisha muswada huo Bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza S. Johari, amesema mabadiliko hayo yanalenga kuboresha utekelezaji wa sheria hizo huku yakiendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Baada ya kupitishwa na Bunge, muswada huo utapelekwa kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua zaidi za kisheria.

Mabadiliko hayo yakikamilika, sheria hizo zitaanza kutumika kwa kuzingatia masharti mapya na utaratibu wake elekezi.