Dkt. mwigulu atoa wito wa maandalizi ya mapema kukabili athari za el niño

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Watanzania na viongozi katika ngazi zote kuchukua tahadhari na kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazohusishwa na hali ya El Niño. 

Dkt. Mwigulu ametoa rai hiyo leo, Jumapili, Septemba 6, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Ilongero, Wilaya ya Singida, mkoani Singida, katika ziara yake ya kikazi ya kusikiliza kero za wananchi na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema maeneo yenye historia ya mafuriko yanapaswa kutambuliwa mapema na hatua za tahadhari kuchukuliwa, huku akiwataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi kuzingatia taarifa na maelekezo ya mamlaka husika. “Maeneo ambayo mnaona ni ya hatari sana Watanzania tunayajua. Tunayajua maeneo yenye historia ya mafuriko. Ni vyema tukaanza kuchukua tahadhari kwa sababu hicho ndicho tunachoweza kukifanya,” amesema.

Kuhusu barabara ya Igauri–Ilongero, Dkt. Mwigulu ameagiza ndani ya Septemba mchakato wa kumpata mkandarasi wa ujenzi wa kilomita 11 za awali ukamilike ili ujenzi uanze haraka. Amesema fedha za mradi huo zipo na kinachosubiriwa ni kumpata mkandarasi. “Ndani ya mwezi huu huu, muwe mmeshatangaza kupata mkandarasi wa kuanza kujenga hizi kilomita 11 za awali ambazo zitaziba hili pengo kuanzia hapa mpaka kwenye lami na kupita kidogo mji wa Ilongero,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha zinazookolewa katika maeneo ya kipaumbele, hususan elimu, afya, maji na miundombinu. Amesema Serikali inapaswa kuanza mapema maandalizi ya madarasa, maabara na maktaba kutokana na ongezeko la wanafunzi wanaotarajiwa kuingia kidato cha kwanza kuanzia mwaka 2028.

Kuhusu afya, Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa ambulensi zinapaswa kuwa tayari muda wote na kuwa na mafuta ili wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura na rufaa wasicheleweshwe. Aidha, amewataka Watanzania kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, akisema mfumo huo utasaidia kupunguza utegemezi wa michango ya dharura wakati wananchi wanapokabiliwa na gharama za matibabu.

Kuhusu maji, Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji na umwagiliaji kwa ushirikiano wa wizara zinazohusika, ili kunufaisha wananchi, mifugo na shughuli za uzalishaji. Amesema Serikali itaendelea kusimamia matumizi yenye tija ya rasilimali za umma na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha, ufanisi na mahitaji halisi ya wananchi.