Dkt. Mwigulu: ndani ya wiki moja tutachukua hatua kushusha bei ya saruji


BARIADI, SIMIYU.

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema ndani ya wiki moja Serikali itachukua hatua kuhakikisha bei ya saruji inakuwa himilivu kwa wananchi, baada ya kubaini malalamiko ya kupanda kwa bei katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Simiyu.

Ametoa kauli hiyo jana, Jumanne Septemba 15, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Bariadi Mjini katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya CCM Saba Saba, akisema Serikali imewatuma wataalamu kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo. Amesema katika baadhi ya maeneo mfuko wa saruji umefikia zaidi ya Sh26,000, huku mikoa ya mipakani ukifikia Sh32,000.

Kuhusu zao la pamba, Dkt. Mwigulu amesema ameielekeza Wizara ya Kilimo kukutana na wadau ndani ya mwezi mmoja na ifikapo Oktoba 15, 2026 kuwasilisha mapendekezo kuhusu bei na mfumo bora wa ununuzi wa pamba, ili kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali imebadili utaratibu wa kodi kwa biashara mpya, ambapo wafanyabiashara wanaoanzisha biashara watapewa mwaka mmoja wa kuimarisha shughuli zao kabla ya kuanza kubeba mzigo wa kodi. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050 inayolenga kujenga uchumi shirikishi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Bariadi Mjini na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrea Mathew, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria wenye thamani ya Sh440 bilioni, ujenzi wa daraja la Majaida–Munambala wenye thamani ya Sh460 milioni kupitia TARURA, pamoja na soko la kisasa la Bariadi.

Amesema pia Serikali imepanga kujenga kilomita 8.6 za barabara za Bariadi Mjini kwa awamu mbili, ambapo kilomita tano zitajengwa katika awamu ya kwanza. Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, amesema mkoa utatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji Ofisi ya Waziri Mkuu.