Mama Janeth Magufuli kutembelea Makumbusho ya Taifa, ujumbe wa urithi wazidi kusikika


DAR ES SALAAM, 15 SEPTEMBA 2026. 

Ziara ya Mama Janeth Magufuli katika Makumbusho ya Taifa imeongeza hamasa ya kutembelea maeneo ya urithi na kujifunza historia, utamaduni na kumbukumbu muhimu za Taifa la Tanzania.

Mama Janeth Magufuli, ambaye ni mke wa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ametembelea maeneo mbalimbali ya Makumbusho ya Taifa na kujionea maonesho ya vitu na kumbukumbu za kihistoria vinavyohifadhiwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Katika ziara hiyo, Mama Janeth amepata fursa ya kuona na kujifunza kuhusu baadhi ya vitu vya urithi vinavyohifadhiwa katika Makumbusho hayo, ikiwemo ndege ya kihistoria aina ya Fokker F28 Fellowship yenye usajili 5H-CCM, ambayo ni sehemu ya kumbukumbu za historia ya uongozi na maendeleo ya Tanzania.

Ziara hiyo imeendelea kuonesha umuhimu wa kuhifadhi na kuthamini urithi wa Taifa, ikizingatiwa kuwa vitu vya kihistoria na kumbukumbu vilivyohifadhiwa katika Makumbusho ni sehemu ya utambulisho wa Taifa na chanzo muhimu cha elimu kwa vizazi mbalimbali.

Aidha, ziara hiyo inatoa hamasa kwa wananchi, hususan familia, vijana na wanafunzi, kutumia fursa zilizopo kutembelea Makumbusho ya Taifa ili kujifunza historia ya Tanzania, kufahamu utamaduni wa jamii mbalimbali na kutambua thamani ya urithi wa Taifa.

Makumbusho ya Taifa yanaendelea kuwakaribisha wananchi na wageni kutoka ndani na nje ya Tanzania kutembelea maeneo yake mbalimbali, kujifunza na kushiriki katika juhudi za kuhifadhi na kuendeleza urithi wa Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.



#TumerithisishwaTuwarithishe