Geita yashuhudia mapinduzi jikoni kupitia majiko ya TANESCO




GEITA.

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limepeleka teknolojia ya majiko ya kisasa yanayotumia umeme katika Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.

Katika maonesho hayo, TANESCO linaonyesha majiko ya Pressure Cooker na Induction yanayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kupunguza utegemezi wa kuni.
Afisa Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Geita, Lucas Sweet Sweke, amesema majiko hayo yanapika kwa haraka, yanatumia umeme kwa ufanisi na hayatoi moshi, hivyo kuwa fursa kwa wananchi kuachana na matumizi ya kuni.

Amesema wananchi wanaotembelea banda la TANESCO wanapata elimu ya moja kwa moja kuhusu matumizi ya majiko hayo na kuyaona yakifanya kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Louis Peter Bura, ambaye alitembelea banda hilo Septemba 29, 2026, amewataka wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona changamoto katika miundombinu ya umeme, badala ya kusubiri umeme ukatike.

Bura amesema wananchi wanapaswa kutoa taarifa wanapoona nguzo imeegama, waya umeanguka au shughuli za uchimbaji zikifanyika karibu na nguzo, akisisitiza kuwa kulinda miundombinu ya umeme ni kulinda maendeleo ya jamii.

Pia amepongeza mfumo wa kidijitali unaotumiwa na TANESCO kupitia vikundi vya WhatsApp, akisema umewezesha wananchi kuwasilisha kero zao bila kulazimika kufika ofisini na hivyo kuchangia kupunguza malalamiko.

Aidha, Bura amesema matumizi ya nishati safi yanapaswa kwenda sambamba na utunzaji wa mazingira, akieleza kuwa matumizi ya majiko yanayotumia umeme yanaweza kusaidia kupunguza ukataji wa miti na kulinda mazingira.