Ratiba ya Mitihani ya Taifa yabadilishwa kuepuka El Niño


DAR ES SALAAM. 

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), imebadilisha ratiba ya baadhi ya mitihani na upimaji wa kitaifa kwa Darasa la Nne, Darasa la Pili, Kidato cha Pili na Kidato cha Nne, iliyokuwa ifanyike Novemba 2026, na sasa sehemu kubwa itafanyika kuanzia Oktoba 2026.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Ameir Hafidh, amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kuzingatia utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), unaoonesha uwezekano wa mvua za El Niño kuanza Oktoba na kuongezeka Novemba 2026.

Amesema hatua hiyo pia imezingatia maelekezo ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya kuchukua tahadhari mapema, ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu na wasimamizi, pamoja na kuwezesha mitihani kufanyika katika mazingira salama na yenye utulivu.

Kwa mujibu wa Wizara, kuendelea na ratiba ya awali kungeweza kusababisha changamoto katika usafirishaji wa vifaa na nyaraka za mitihani kutokana na uwezekano wa mafuriko na uharibifu wa miundombinu ya barabara, huku wanafunzi na wasimamizi wakikabiliwa na uwezekano wa kuchelewa kufika vituoni.

Aidha, Wizara imesema mvua kubwa zinaweza kuathiri upatikanaji wa umeme na huduma za mawasiliano katika baadhi ya maeneo, pamoja na kuongeza changamoto za kiafya na usafi katika vituo vya mitihani, hasa kwa kuzingatia usalama wa wanafunzi wadogo.

Akizungumzia ratiba mpya, Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said A. Mohamed, amesema Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA) utafanyika Oktoba 5 na 6, 2026, huku Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili (STNA) ukifanyika Oktoba 7 na 8, 2026.

Amesema Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA) utafanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 23, 2026, wakati Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne (CSEE) utafanyika kuanzia Oktoba 19 hadi Novemba 6, 2026.

Profesa Mohamed amewataka wadau wa elimu, wakiwemo Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri, wakuu wa shule, walimu, wazazi na wanafunzi, kufanya maandalizi kwa kuzingatia ratiba hiyo mpya.

Wizara imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote katika kuhakikisha mitihani na upimaji huo unafanyika kwa usalama, utulivu na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Ratiba rasmi pamoja na maelekezo zaidi vinapatikana kupitia tovuti rasmi ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA).