DAR ES SALAAM
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limebaini matukio ya wizi wa umeme katika maeneo ya Visiwani, Mwananyamala na Mivumoni, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, wakati wa operesheni ya ukaguzi wa mita na miundombinu ya umeme inayoendelea katika Mkoa huo.
Operesheni hiyo inalenga kudhibiti matumizi yasiyo halali ya umeme, kulinda miundombinu ya Shirika na kuhakikisha huduma ya umeme inaendelea kutolewa kwa usalama na ufanisi kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo, Afisa Usalama wa TANESCO, Bi. Lilian Nizim, amewataka wananchi kuzingatia sheria na taratibu za matumizi ya umeme na kuepuka kuingilia au kuchezea mita. Amesema mteja anayebaini changamoto yoyote kwenye mita yake anapaswa kutoa taarifa TANESCO ili ipatiwe ufumbuzi.
Kwa upande wake, Mhandisi wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kaskazini, Mha. Underson Manyika, amesema ukaguzi katika eneo la Visiwani umebaini baadhi ya wateja wamechepusha nyaya za umeme, hali iliyosababisha mita kutosoma matumizi halisi ya umeme.
Mha. Manyika amesema miunganisho hiyo isiyo halali inaathiri usomaji sahihi wa mita na kwamba hatua stahiki zinaendelea kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za Shirika. Ameongeza kuwa vitendo vya wizi wa umeme husababisha hasara kwa Shirika, kuhatarisha usalama wa wananchi na kuathiri ubora wa huduma.
TANESCO imewataka wananchi kushirikiana na Shirika kwa kutoa taarifa za vitendo vya wizi wa umeme, huku ikisisitiza kuwa ukaguzi wa mita na miundombinu utaendelea katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuhakikisha huduma ya umeme inakuwa ya uhakika, salama na endelevu.
#TANESCO #WiziWaUmeme #Umeme #Kinondoni #DarEsSalaam


