Tanzania imeandika historia katika mashindano ya urembo duniani baada ya mwakilishi wake, Jihan Dimack, kutwaa taji la Miss Grand International 2026 yaliyofanyika Bangkok, Thailand, Oktoba 10, 2026. Ushindi huo umeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kupata taji hilo.
Jihan amefanikiwa kuibuka mshindi akiwashinda washiriki kutoka mataifa mbalimbali, huku mwakilishi wa Ecuador, Shyare Andrade, akishika nafasi ya pili na Beau Megan Goos wa Uholanzi akimaliza katika nafasi ya tatu.
Katika hatua ya maswali na majibu, Jihan alisisitiza umuhimu wa mwanamke mwenye moyo wa upendo na wema, akimtaja mama yake kama mfano wa mwanamke anayewajali wengine na kuweka mahitaji yao mbele.
Ushindi huo ni hatua muhimu kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, kwani unaongeza utambulisho wa bara hilo katika mashindano ya kimataifa ya urembo.
Jihan, ambaye ana asili ya Kitanzania na Lebanon, aliwahi kushiriki mashindano ya Miss Universe Tanzania mwaka 2016 na kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss Universe yaliyofanyika Ufilipino mwaka 2017.
Kwa ushindi huo, Jihan anaingia katika historia ya Miss Grand International akiwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kutwaa taji hilo tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.
