Na Mwandishi wetu, Njombe
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Wilaya ya Njombe, imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja kwa lengo la kurahisisha usafiri na wananchi kufikia huduma za kijamii.
Meneja wa TARURA Njombe, Mhandisi Costantine Ibengwe, amesema miongoni mwa miradi inayoendelea ni ujenzi wa barabara ya NBC-Kibena kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 2.84.
Pia, ujenzi wa daraja la mawe lenye urefu wa mita 31 linalounganisha Kata za Mji Mwema na Ramadhani umefikia asilimia 70.
Barabara ya Mama White yenye urefu wa kilomita 1.5 kwa kiwango cha changarawe imekamilika na tayari inatumika. Kwa mujibu wa Mhandisi Ibengwe, barabara hiyo imerahisisha wananchi kufikia barabara kuu ya Songea, Ofisi za Mkuu wa Mkoa na Kituo cha Afya cha Mji Mwema.
“Tunatekeleza miradi hii ili kuwawezesha wananchi kusafiri kwa urahisi na kufanya shughuli zao za kila siku bila shida,” amesema Mhandisi Ibengwe.
Wakati huohuo, Mkazi wa Njombe, Maulus Mlowe, ameipongeza TARURA akisema barabara hiyo imeondoa changamoto ya usafiri na kurahisisha pia wanafunzi kufika maeneo mbalimbali.
“Zamani eneo hili lilikuwa halipitiki, ila sasa imekuwa njia rahisi kwetu na wanafunzi wanapita kwa urahisi,” amesema Mlowe.

