Na Charles Mkoka
Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Omar Ali Shetta, ameeleza uzoefu wake wa kuishi katika Bonde la Mto Msimbazi, akisisitiza madhara makubwa ya mafuriko yaliyodumu kwa miaka mingi, huku akieleza matumaini mapya yanayotokana na mradi wa maboresho unaoendelea.
Akizungumza katika hafla ya mradi huo, Shetta alisema ameshuhudia binafsi changamoto zilizokuwa zikikumba wakazi wa eneo hilo, ikiwemo vifo, uharibifu wa nyumba na upotevu wa mali.
“Tumeshuhudia watu wakipoteza maisha, nyumba kujaa maji na mali kuharibika. Hali hii ilikuwa kama jambo la kawaida kwa wakazi wa maeneo haya,” alisema.
Mradi huo unahusisha maboresho ya usimamizi wa maji, udhibiti wa mafuriko pamoja na ujenzi wa miundombinu, ukilenga kubadilisha maisha ya wakazi wa Ilala na maeneo jirani.
Aidha, utekelezaji wa miradi ya barabara za mitaa ikiwemo Kanyenge na Talula unatarajiwa kuboresha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.
Meya huyo alisema viongozi wa serikali za mitaa wameonesha mshikamano mkubwa katika kuunga mkono mradi huo, wakiahidi kushirikiana kikamilifu na serikali kuu ili kuhakikisha unatekelezwa kwa mafanikio.
Alitoa pia shukrani kwa viongozi wa kitaifa kwa kuanzisha mradi huo, akisema unaashiria dhamira ya kuboresha maisha ya wananchi na kuleta maendeleo ya kudumu.
Wananchi wa maeneo husika wameeleza matumaini makubwa kuwa mradi huo utasaidia kuondoa changamoto za kijamii na kiuchumi zilizodumu kwa muda mrefu.
Mradi huo unatarajiwa kupunguza athari za mafuriko na kufungua fursa mpya za maendeleo ya biashara, utalii na ukuaji wa jiji la Dar es Salaam
0 Comments