Dkt. Mwinyi akaribisha wawekezaji wa Uturuki kuwekeza Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na Balozi Volkan Isikei, ambaye ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Uturuki, akiwa pamoja na ujumbe wake akiwemo Balozi wa Uturuki, Mhe. Dkt. Bekir Gezer, walipofika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya mazungumzo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu, tarehe 2 Mei, 2026.

Na Mwandishi wetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa wito kwa makampuni na wawekezaji kutoka Uturuki kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo nchini, hususan katika sekta za biashara, nishati na miundombinu.

Rais Mwinyi aliyasema hayo leo, Mei 2, 2026, Ikulu Zanzibar alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki, Balozi Volkan Isikci, aliyefuatana na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Bekir Geze.

Katika mazungumzo hayo, Rais Mwinyi alisema mikutano ya aina hiyo inaendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Uturuki, huku ikifungua milango ya fursa mpya za ushirikiano, hasa katika nyanja za biashara na uwekezaji.

Alieleza kuwa huu ni wakati muafaka kwa wawekezaji wa Uturuki kuwekeza katika miradi ya kimkakati ikiwemo madini, kilimo, utalii, afya na miundombinu, akibainisha kuwa Tanzania ina mazingira rafiki ya uwekezaji.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini badala ya kuziuza kama malighafi. Alitolea mfano mazao ya korosho, chai na kahawa ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakisafirishwa nje bila kuchakatwa kikamilifu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, akisalimiana na Balozi Volkan Isikei, ambaye ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Uturuki, alipofika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya mazungumzo katika Ukumbi wa Ikulu, tarehe 2 Mei, 2026.

Akizungumzia sekta ya nishati, Rais Mwinyi alisema Zanzibar inaendelea na jitihada za kufikia umeme wa kujitegemea, akieleza kuwa eneo hilo lina fursa kubwa kwa wawekezaji wa kimataifa. Pia alitaja uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji uwekezaji.

Sambamba na hayo, Rais Mwinyi aliipongeza Uturuki kwa mchango wake katika maendeleo ya Tanzania, ikiwemo Zanzibar, kupitia miradi ya elimu, afya, kilimo na miundombinu pamoja na utoaji wa mafunzo kwa Watanzania, akisisitiza haja ya kuimarisha zaidi ushirikiano huo.

Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Bekir Geze, alisema uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ni wa kirafiki na wa muda mrefu, akisisitiza kuwa wakati umefika wa kuupanua zaidi kupitia biashara na uwekezaji.

Naye Balozi Volkan Isikci aliahidi kuendeleza na kuimarisha ushirikiano kati ya Uturuki na Tanzania kupitia mkakati wa nchi yake wa kusaidia maendeleo ya mataifa ya Afrika, akibainisha kuwa ushirikiano huo utagusa sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, kilimo, miundombinu na utalii.

Mkutano huo unaonekana kuwa hatua muhimu katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kuimarisha mahusiano ya kimkakati kati ya Tanzania na Uturuki.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, akikabidhiwa zawadi na Balozi Volkan Isikei, ambaye ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Uturuki, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu, tarehe 2 Mei, 2026.


Post a Comment

0 Comments