Bilionea wa Tanzania Mohammed Dewji ameanza mpango mpya wa kupanua biashara ya vinywaji Afrika Mashariki baada ya kutangaza uwekezaji wa zaidi ya Tshs bilioni 130 kwa ajili ya kujenga kiwanda cha soda nchini Kenya.
Kupitia kampuni yake ya MeTL Group, Dewji anatarajia kujenga kiwanda hicho katika mji wa Mombasa huku akilenga kuingia moja kwa moja kwenye ushindani dhidi ya kampuni kubwa za Coca-Cola na Pepsi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya biashara Afrika, kiwanda hicho kitazalisha vinywaji vya Mo Cola, Mo Xtra na Mo Malto ambavyo tayari vimepata soko kubwa Tanzania kwa kuuza bidhaa kwa bei nafuu.
Dewji amesema mradi huo bado uko kwenye hatua za maandalizi lakini ujenzi unaweza kuanza ndani ya miezi 12 ijayo.
Katika miaka ya karibuni, Mo Cola imekuwa moja ya soda zinazouzwa kwa wingi Tanzania huku kampuni hiyo ikitumia mbinu ya bei ya chini kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Ripoti ya Business Daily ya Kenya imeeleza kuwa MeTL inapanga kuuza chupa ya Mo Cola kwa takribani Sh15 za Kenya, sawa na karibu Tshs 300 za Tanzania, kiwango kilicho chini sana ukilinganisha na soda nyingi zinazouzwa nchini humo.
Hatua hiyo inatajwa kuongeza ushindani mkubwa katika soko la vinywaji Afrika Mashariki ambalo kwa muda mrefu limeongozwa na Coca-Cola pamoja na Pepsi.
Kenya ni moja ya masoko makubwa ya vinywaji ukanda wa Afrika Mashariki, huku kampuni mbalimbali zikizidi kuongeza uwekezaji kutokana na ongezeko la idadi ya watu na matumizi ya bidhaa za haraka.
Mbali na Kenya, Dewji amesema MeTL pia inaendelea na mipango ya kujenga kiwanda kingine cha vinywaji nchini Uganda.
Wachambuzi wa biashara wanasema hatua ya kampuni za Tanzania kuwekeza zaidi nje ya nchi inaonyesha ukuaji wa mtaji wa ndani pamoja na uwezo wa kampuni za Afrika Mashariki kushindana kimataifa.
Mo Dewji ni mmoja wa wafanyabiashara wakubwa Afrika na kwa mujibu wa Forbes anatajwa kuwa mmoja wa matajiri wakubwa zaidi barani humo.
