Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameyakaribisha makampuni na wawekezaji kutoka Uturuki kuwekeza nchini, hususan katika maeneo ya biashara, nishati na miundombinu.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 02 Mei 2026, alipokutana na Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, Balozi Volkan Isikci, akiambatana na mwenyeji wake Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Balozi Bekir Geze, waliofika Ikulu, Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi amesema vikao vya aina hiyo vinaimarisha uhusiano wa muda mrefu baina ya nchi hizo mbili na kutoa fursa mpya katika maeneo mapya ya ushirikiano, hususan masuala ya biashara na uwekezaji. Ameeleza kuwa huu ni wakati sahihi kwa wawekezaji wa Uturuki kuja kuwekeza katika miradi ya madini, kilimo, utalii, afya na miundombinu.
Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikinunua chuma kutoka Uturuki, hivyo ni vema kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa nchi hiyo kuwekeza Tanzania na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini, ikiwemo korosho, chai na kahawa ambazo zimekuwa zikiuzwa kama malighafi.
Amesema Zanzibar inafanya juhudi kubwa za kuwa na umeme wa kujitegemea na kwamba eneo hilo lina fursa kubwa ya uwekezaji. Hivyo, ni vema wawekezaji wa Uturuki wakatumia fursa hiyo pamoja na eneo la uimarishaji wa viwanja vya ndege kuja kuwekeza.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesifu misaada inayotolewa na nchi hiyo kwa Tanzania, ikiwemo Zanzibar, katika sekta za elimu, afya, kilimo na miundombinu, pamoja na fursa za mafunzo nchini humo, na kusisitiza kuongezwa zaidi.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mkurugenzi huyo, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Balozi Bekir Geze, amesema mataifa hayo ni rafiki na kueleza kuwa ni wakati wa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano na kufanya kazi pamoja, hususan katika eneo la biashara na uwekezaji.
Naye Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika, Balozi Volkan Isikci, ameihakikishia Tanzania, ikiwemo Zanzibar, ushirikiano zaidi kupitia mkakati wa nchi hiyo kwa maendeleo ya nchi za Afrika, ili kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi katika nyanja mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, kilimo, miundombinu na utalii.
#Uturuki #Tanzania #Zanzibar
0 Comments