Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimefungua dirisha la udahili kwa mwaka wa masomo 2026/27 na kuwataka vijana wa Tanzania kutumia fursa zinazozidi kuongezeka katika sekta ya bahari na uchumi wa buluu.
Chuo hicho kwa sasa kinapokea maombi ya wanafunzi wa ngazi ya cheti, diploma, shahada na shahada za uzamili, pamoja na kozi mbalimbali za kitaaluma za mabaharia kuanzia ngazi za awali hadi maofisa wa meli.
Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Mwisila Lucas, amesema Tanzania inaendelea kuwekeza katika sekta ya bahari, hali inayofungua nafasi zaidi za ajira na ujasiriamali kwa vijana.
"Kozi zetu zinamwezesha mhitimu kuajiriwa lakini pia kujiajiri. Sekta ya bahari bado ina fursa nyingi ambazo vijana wanapaswa kuzitumia," amesema.
Profesa Lucas amesema Serikali imeendelea kukiimarisha chuo hicho kwa kukipatia vifaa vya kisasa vya mafunzo ya uhandisi wa bahari, urubani wa meli, usafirishaji na ushughulikiaji wa mizigo bandarini pamoja na maeneo mengine muhimu ya sekta hiyo.
Amesema chuo pia kimeongeza wataalamu katika nyanja mbalimbali zikiwemo uhandisi wa bahari, unahodha wa meli, uchumi wa bahari, sheria za bahari na usimamizi wa shughuli za majini ili kuhakikisha kinazalisha wahitimu wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Mbali na mafunzo, chuo kinatoa huduma za ushauri elekezi kwa taasisi za umma na binafsi zinazojihusisha na shughuli za baharini pamoja na kufanya tafiti zinazochangia maendeleo ya uchumi wa buluu nchini.
Profesa Lucas amesema ushiriki wa DMI katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kutoa elimu kuhusu fursa zinazopatikana katika sekta ya bahari.
"Tunatoa elimu kuhusu mafunzo yetu, ushauri elekezi na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya bahari. Wananchi wanaweza kufika banda letu na kupata maelezo ya moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wetu," amesema.
Amesema dirisha la kwanza la udahili linatarajiwa kufungwa Julai 10 mwaka huu na amewahimiza wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na sita pamoja na wazazi kutembelea tovuti ya chuo hicho ili kupata taarifa za kozi na vigezo vya kujiunga.
Aidha, amesema wanafunzi watakaodahiliwa wanaweza kunufaika na fursa mbalimbali za mikopo na ufadhili kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), mfuko wa mikopo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mfuko wa Samia Scholarship pamoja na mifuko mingine inayosaidia wanafunzi wa sekta ya bahari.
Kadri Tanzania inavyoendelea kuwekeza katika uchumi wa buluu, sekta za usafiri wa majini, bandari, uvuvi, huduma za baharini na biashara zinazohusiana na bahari zinatajwa kuwa miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kuzalisha ajira nyingi zaidi katika miaka ijayo.
