Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ametembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alipata fursa ya kujionea huduma na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Mfuko huo kwa manufaa ya Wafanyakazi na wategemezi wao.
Katika ziara hiyo fupi, Dkt. Kiruswa alielezwa kuhusu nafasi ya WCF katika kulinda ustawi wa nguvukazi ya Taifa kwa kutoa fidia kwa wafanyakazi wanaopata ajali au ugonjwa unaotokana na kazi.
Aidha, Mhe. Naibu Waziri alijionea huduma mbalimbali zinazotolewa kidijitali na Mfuko huo kwa waajiri na wafanyakazi.
Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya Kongamano la Madini linalofanyika sambamba na Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.
WCF inaendelea kuwakaribisha Wadau wote kutembelea banda lake lililopo katika viwanja hivyo ili kupata elimu na uelewa wa kina kuhusu huduma zake, zikiwemo usajili wa waajiri, ulipaji wa michango kwa njia ya mtandao, utoaji wa taarifa za ajali na magonjwa yatokanayo na kazi, ufuatiliaji wa madai ya fidia, huduma za matibabu, fidia ya ulemavu wa muda na wa kudumu, na huduma za utengemao (rehabilitation).

