Wananchi: Sabasaba ni zaidi ya maonesho, ni darasa la huduma na biashara


 Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Watembeleaji wa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) wamesema maonesho ya mwaka huu yameendelea kuwa jukwaa muhimu la wananchi kupata huduma, elimu na taarifa kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi.

Mkazi wa Tabata, Diocles Desdery, alisema alifika maoneshoni kwa lengo la kujionea huduma na bidhaa mpya huku akibainisha kuwa hali ya usalama ilikuwa nzuri tangu alipoondoka nyumbani hadi alipowasili viwanjani.

"Nimezunguka kwenye mabanda mbalimbali na kila kitu kinaendelea vizuri. Hakuna changamoto yoyote ya usalama niliyoiona," alisema.

Aliwahimiza wananchi wenye hofu kujitokeza kutembelea maonesho hayo, akisema mazingira ni salama na kuna mengi ya kujifunza.


Naye Khalid Hassani alisema kila anapotembelea Sabasaba hupata maarifa mapya kuhusu huduma, bidhaa na fursa mbalimbali zinazotolewa na waoneshaji.

"Sabasaba ni sehemu ya kujifunza. Kuna mambo mengi ambayo huwezi kuyapata mahali pengine kwa wakati mmoja. Ninawaomba Watanzania wajitokeze kushiriki maonesho haya," alisema.

Aliongeza kuwa usalama umeimarishwa na wageni wanaendelea kutembelea mabanda mbalimbali kwa utulivu huku wakipata huduma na elimu kutoka taasisi zinazoshiriki maonesho hayo.

Maonesho ya Sabasaba yameendelea kuvutia maelfu ya wananchi wanaofika kujionea bidhaa, huduma, ubunifu na fursa za uwekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania.