Wananchi wasifu usalama na huduma zinazotolewa Sabasaba 2026

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Baadhi ya wananchi waliotembelea Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) wamewahamasisha Watanzania kujitokeza kutembelea maonesho hayo, wakisema hali ya usalama ni nzuri na shughuli zote zinaendelea kama kawaida.

Mkazi wa Zanzibar, Makame Khamis Mohamed, alisema alifika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba) mapema na kushuhudia shughuli zikiendelea kwa utulivu bila changamoto za kiusalama.

Alisema wananchi wasiwe na hofu ya kutembelea maonesho hayo kwa kuwa huduma mbalimbali zinaendelea kutolewa na waoneshaji kutoka taasisi za umma na sekta binafsi.

"Nimetoka Zanzibar na nimekuta mazingira ni salama. Nawaomba wananchi wajitokeze kutumia fursa hii kupata huduma, bidhaa na elimu inayotolewa na taasisi mbalimbali," alisema.

Kwa upande wake, Mohammed Yomari Tego, mkazi wa Mbagala, alisema ametembelea mabanda mbalimbali na kujionea huduma zinazotolewa huku akieleza kuwa hakushuhudia hali yoyote isiyo ya kawaida.

Alisema maonesho hayo yamekusanya taasisi nyingi zinazotoa huduma muhimu ikiwemo usajili wa vitambulisho, huduma za kifedha na taarifa mbalimbali za serikali.

"Nawaomba wananchi ambao bado hawajafika waje. Kuna huduma nyingi muhimu zinazopatikana sehemu moja na mazingira ni salama," alisema.

Maonesho ya Sabasaba 2026 yanaendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13.