Na Charles Mkoka
Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma Zinazodhibitiwa na EWURA (EWURA CCC) linatumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026) kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki za watumiaji pamoja na matumizi salama ya umeme, maji na gesi ya kupikia (LPG).
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Mwandamizi Uelimishaji na Uhamasishaji wa EWURA CCC, Lugiko L. Lugiko, alisema lengo ni kuwajengea wananchi uelewa sahihi kuhusu haki na wajibu wao wanapotumia huduma zinazodhibitiwa na EWURA ili waweze kufanya maamuzi sahihi.
Alisema baraza hilo linaendelea kutoa elimu kuhusu sekta za umeme, mafuta, gesi asilia pamoja na huduma za maji na usafi wa mazingira.
"Mtumiaji mwenye taarifa sahihi ndiye mtumiaji mwenye uwezo wa kufanya maamuzi bora. Tunataka wananchi wajue haki zao lakini pia wajibu wao wanapotumia huduma hizi," alisema Lugiko.
Aliwataka watumiaji wa umeme kuhakikisha kazi zote za ufungaji wa mfumo wa umeme zinafanywa na mafundi wenye leseni kutoka EWURA ili kupunguza hatari za ajali na kuhakikisha mifumo inakuwa salama.
Pia aliwashauri wananchi kutumia vifaa vya umeme vilivyoidhinishwa na kukagua mifumo ya umeme majumbani angalau kila baada ya miaka mitano ili kupunguza matumizi makubwa ya umeme, uharibifu wa vifaa na hatari za moto.
Kuhusu huduma za maji, Lugiko alisema wananchi wanaopata bili kubwa zisizo za kawaida wanapaswa kwanza kuhakiki usomaji wa mita zao na kukagua kama kuna uvujaji wa maji kabla ya kuwasilisha malalamiko kwa mamlaka husika.
"Wakati mwingine bili kubwa haitokani na makosa ya mamlaka ya maji, bali uvujaji wa maji ndani ya nyumba au kutokufuatilia usomaji wa mita," alisema.
Kwa upande wa matumizi ya gesi ya kupikia (LPG), aliwataka wananchi kusafirisha mitungi ikiwa imesimama wima na kuihifadhi katika maeneo yenye hewa ya kutosha ili kupunguza hatari ya uvujaji wa gesi.
Alisema EWURA CCC itaendelea kupanua kampeni za elimu kwa umma ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kutumia huduma za nishati na maji kwa usalama, ufanisi na kuzingatia sheria.
