Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Rhimo S. Nyansaho, ameipongeza SUMA JKT kwa kuendelea kutoa ajira kwa maelfu ya vijana na kupanua huduma zake, akisema taasisi hiyo imekuwa nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya uchumi na kuwawezesha vijana kujiajiri.
Dk. Nyansaho amesema hayo baada ya kutembelea banda la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026).
Alisema ushiriki wa JKT kwenye maonesho hayo umewapa wananchi nafasi ya kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo pamoja na programu za mafunzo ya ufundi na stadi za kazi zinazowajengea vijana uwezo wa kujitegemea.
"JKT siyo tu inajenga uzalendo kwa vijana, bali pia inawapatia ujuzi unaowasaidia kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa," alisema Dk. Nyansaho.
Alitaja shughuli za SUMA JKT, ikiwemo huduma za kudhibiti wadudu waharibifu (fumigation), kuwa miongoni mwa miradi inayochangia kutoa ajira, huku kampuni hiyo ikiwa imeajiri takribani vijana 4,800 nchini.
Dk. Nyansaho alisema wananchi waliotembelea banda hilo wamepata fursa ya kufahamu huduma nyingi zinazotolewa na JKT ambazo hazifahamiki kwa wengi, pamoja na mchango wa taasisi hiyo katika maendeleo ya vijana na uchumi wa taifa.
Aidha, aliupongeza uongozi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na JKT kwa kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi sambamba na kuanzisha miradi inayozalisha ajira na kuongeza kipato kwa vijana.
