Na Charles Mkoka, Dar es Salaam
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Dk. Evaline Munisi, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika maendeleo ya ujuzi wa Watanzania ili kujenga wataalamu wa ndani na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.
Dk. Munisi amesema hayo baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026).
Alisema maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kupata elimu kuhusu ajira, mahusiano kazini, usalama na afya mahali pa kazi, fidia kwa wafanyakazi pamoja na huduma za hifadhi ya jamii.
"Ndani ya miaka michache ijayo hatutakuwa tena na utegemezi mkubwa wa wataalamu kutoka nje, kwa sababu tunawaandaa wataalamu wetu hapa nchini. Huu ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga nguvu kazi yenye ujuzi na ushindani," alisema Dk. Munisi.
Alisema kuwa ameridhishwa na maendeleo ya programu za mafunzo ya ujuzi alizozitembelea hivi karibuni, akibainisha kuwa zitasaidia vijana kuhimili ushindani katika soko la ajira linalobadilika kutokana na maendeleo ya teknolojia.
Aidha, aliwapongeza watumishi wa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuboresha utoaji wa huduma na kutumia mifumo ya kidijitali kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Ushirikiano kati ya Serikali, waajiri, wafanyakazi, asasi za kiraia, taasisi za dini na wadau wengine wa maendeleo ni muhimu katika kujenga mazingira bora ya kazi na kuharakisha maendeleo ya taifa.
Katika ziara hiyo alitembelea mabanda ya taasisi mbalimbali, zikiwemo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
Alivutiwa pia na huduma za kidijitali zinazotolewa na NSSF, ambazo zinawawezesha wanachama kupata taarifa za mafao na akaunti zao kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika kwenye ofisi za mfuko huo.
Dk. Munisi amewahimiza wananchi wanaotembelea Sabasaba kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake ili kujifunza kuhusu huduma mbalimbali za Serikali, fursa za ajira na programu zinazotekelezwa kwa maendeleo ya wananchi.
