Zaidi ya wanafunzi 125,000 wafaulu Kidato cha Sita 2026


Na Mwandishi wetu

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita (ACSEE) 2026, yakionyesha kiwango cha ufaulu kikiendelea kuwa cha juu huku zaidi ya asilimia 99 ya watahiniwa wa shule wakifaulu.

Akizungumza baada ya kikao cha 172 cha Baraza kilichofanyika Julai 4, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa NECTA, Prof. Said Mohamed, alisema jumla ya watahiniwa 133,647 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo 126,556 wa shule na 7,091 wa kujitegemea.

Prof. Said alisema kati ya watahiniwa wa shule, 125,320 walifanya mtihani, huku 125,056, sawa na asilimia 99.92, wakifaulu na watahiniwa 97 pekee wakishindwa.

Kwa watahiniwa wa kujitegemea, alisema 6,112, sawa na asilimia 94.50, walifaulu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.80 ikilinganishwa na mwaka 2025.

Katika ubora wa ufaulu, takwimu zinaonyesha watahiniwa 124,603, sawa na asilimia 99.56, walipata madaraja ya I hadi III.

Kati yao, 67,696 walipata Daraja la I, sawa na asilimia 54.09, huku 43,515 wakipata Daraja la II, sawa na asilimia 34.77.

"Kiwango cha ufaulu kwa watahiniwa wa shule kimeendelea kuwa cha juu mwaka 2026, huku ubora wa ufaulu ukiendelea kuimarika," alisema Prof. Said.

Mbali na matokeo ya Kidato cha Sita, NECTA pia imetangaza matokeo ya mitihani ya ualimu kwa mitaala ya zamani na mitaala iliyoboreshwa ya mwaka 2023, ikiwemo Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Msingi, Elimu ya Awali na Elimu Maalumu.

Kwa mujibu wa NECTA, matokeo hayo yanaonyesha mahudhurio ya watahiniwa katika mitihani yote yaliendelea kuwa ya juu, huku idadi kubwa ya watahiniwa wakihudhuria na kukamilisha mitihani yao.