Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb.), amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) umeanza kuzaa matunda, baada ya vifaa vya kisasa vya uchunguzi na tiba kuokoa zaidi ya Sh3.5 bilioni ambazo zingetumika kuwapeleka wagonjwa kutibiwa nje ya nchi.
Akizungumza alipotembelea taasisi hiyo, Zungu alisema jukumu la Bunge ni kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuhakikisha fedha hizo zinarejea kwa wananchi kupitia huduma bora za kijamii.
"Tunapohimiza ukusanyaji wa kodi, lengo ni kuona fedha hizo zinarejea kuwahudumia wananchi. Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuimarisha huduma za afya nchini. Leo Watanzania wanaweza kupata huduma ambazo zamani zilihitaji kwenda nje ya nchi," alisema mhe. Zungu.
Alisema ORCI sasa ina vifaa vya kisasa ikiwemo PET Scan, kinachotumika kubaini seli za saratani mapema, pamoja na mashine ya Radiosurgery, inayotibu baadhi ya saratani kwa kutumia mionzi maalumu bila kufanyiwa upasuaji.
Spika huyo alisema Serikali imewekeza takribani Sh7 bilioni kununua mashine ya Radiosurgery, huku akisisitiza kuwa teknolojia hiyo ni miongoni mwa bora zaidi katika ukanda wa Afrika.
Aidha, alisema ujenzi wa jengo jipya la ORCI unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu, huku fedha zote za mradi zikiwa tayari zimetolewa.
Jengo hilo litakuwa na sehemu maalumu kwa wagonjwa wa kimataifa wanaokuja nchini kwa utalii wa tiba pamoja na eneo la kuhudumia Watanzania wanaotibiwa kupitia bima za afya, mfumo wa kuchangia gharama na misamaha ya matibabu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ORCI alisema tangu kifaa cha PET Scan kilipozinduliwa Januari 2026, tayari wagonjwa zaidi ya 350 wamepata huduma hiyo nchini.
Alisema kama wagonjwa hao wangetibiwa nchini India, Serikali na wananchi wangetumia angalau Sh3.5 bilioni, hivyo ndani ya miezi sita pekee huduma hiyo imeokoa fedha hizo.
"Kwa kipindi cha miezi sita tangu Januari hadi sasa, Serikali imeokoa zaidi ya Sh3.5 bilioni. Tukidumisha kasi hii, kwa mwaka mmoja tutaokoa takribani Sh7 bilioni ambazo zamani zingetumika kutibu wagonjwa nje ya nchi," alisema.
Aliongeza kuwa jengo jipya litakuwa sehemu muhimu ya kuimarisha utalii wa tiba nchini, huku likiendelea kutoa huduma kwa Watanzania wote bila ubaguzi, wawe wanatumia bima, mfumo wa kuchangia gharama au misamaha ya matibabu.
Mradi huo unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za kibingwa za saratani katika Afrika Mashariki, huku ukipunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi na kuokoa fedha za kigeni.
