Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa mafanikio katika ujenzi, matengenezo na ukarabati wa barabara, akisema yameongeza upatikanaji wa huduma na kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.
Prof. Kabudi amesema miradi inayotekelezwa na TARURA imekuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha wananchi kufikia huduma muhimu za afya, elimu, masoko na maeneo ya uzalishaji, huku ikiimarisha usafiri na usafirishaji katika maeneo ya vijijini na mijini.
Ameyasema hayo alipotembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.
Akiwa katika banda la TARURA, Prof. Kabudi alijionea utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na matumizi ya teknolojia mbadala katika ujenzi na matengenezo ya barabara.
Amesema ubunifu huo unasaidia kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi, kupunguza gharama za ujenzi na kuhakikisha wananchi wanapata miundombinu bora, salama na inayodumu kwa muda mrefu.
