TTB yampa Khalid Al Barwani jukumu la kuitangaza Tanzania kimataifa

 Na Mwandishi wetu 

Mwanautalii na mtangazaji wa vivutio vya utalii kutoka Oman, Khalid Hamed Al Barwani, amekabidhiwa rasmi hadhi ya Balozi wa Hiari wa Utalii wa Tanzania, hatua inayolenga kuimarisha kampeni za kuitangaza Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Hadhi hiyo ilikabidhiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ikiwa ni kutambua mchango wa Al Barwani katika kuitangaza Tanzania kupitia majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

Al Barwani alipata umaarufu nchini baada ya kuongoza kundi la Dream Team Explorers kutembelea Shamba la Miti Sao Hill mwaka 2024, ambapo alionesha mandhari ya misitu, Mto Ruaha na vivutio vingine kupitia mitandao ya kijamii, hatua iliyoongeza mwonekano wa eneo hilo kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.

TTB imesema uteuzi huo ni sehemu ya mkakati wa kushirikisha wadau na watu wenye ushawishi duniani kuitangaza Tanzania, kuvutia masoko mapya ya utalii na kuongeza ushindani wa sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Mafuru, mabalozi wa hiari wa utalii wana nafasi muhimu ya kufikisha taarifa kuhusu vivutio vya Tanzania kwa mamilioni ya watu duniani na kuchangia ongezeko la idadi ya watalii pamoja na mapato ya sekta ya utalii.

Uteuzi wa Al Barwani unatarajiwa kuongeza nguvu katika kuitangaza Tanzania, hususan vivutio vya utalii wa misitu na ikolojia kama Sao Hill, ambavyo vinaendelea kuvutia watalii kutoka mataifa mbalimbali.