Na Mwandishi wetu
Bagamoyo. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeanza kupokea wageni wa kwanza walionufaika na ofa maalumu ya Sabasaba ya kutembelea vivutio vya utalii wanavyovisimamia.
Safari hiyo ya kwanza ilifanyika katika Magofu ya Kaole, Bagamoyo, ambapo wageni walipata nafasi ya kujifunza historia ya eneo hilo pamoja na urithi wa ustaarabu wa pwani ya Afrika Mashariki.
Washiriki wa ziara hiyo walijumuisha Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali. Wengi wao walieleza kufurahia fursa hiyo wakisema imewawezesha kuona kwa karibu maeneo ya kihistoria ambayo kwa muda mrefu walikuwa wakiyasikia kupitia vitabu na simulizi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhifadhi Mambo Kale II, Veronica Kombe, alisema ofa hiyo inalenga kuwapa wananchi nafasi ya kutembelea vivutio vya utalii kwa gharama nafuu huku wakijifunza historia na umuhimu wa uhifadhi.
Alisema safari inayofuata chini ya ofa hiyo imepangwa kufanyika Julai 11, 2026 katika Msitu wa Asili wa Pugu-Kazimzumbwi.
Kupitia kampeni hiyo ya Sabasaba, TFS inalenga kuhamasisha utalii wa ndani, kuongeza uelewa kuhusu uhifadhi wa rasilimali za asili na kuwafanya wananchi kushiriki zaidi katika kutunza urithi wa taifa.
Ofa hiyo inaendelea kuvutia makundi mbalimbali ya wananchi wanaotaka kujifunza, kuburudika na kutembelea maeneo yenye historia na umuhimu wa kiikolojia nchini.

