Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Zaidi ya Sh5.5 trilioni zimetumika kununua bidhaa na huduma kutoka kwa kampuni za ndani zinazohudumia migodi nchini.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema fedha hizo sasa zinanufaisha zaidi Watanzania badala ya kwenda kwa kampuni za nje.
Alizungumza leo Julai 8 wakati akifungua Kongamano la Madini kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Kwa mujibu wa Dkt. Kiruswa, mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa sera ya ushirikishwaji wa wazawa (Local Content).
Alisema kampuni za Kitanzania sasa zinapata nafasi kubwa zaidi katika zabuni za migodini.
Fedha hizo zimetumika katika sekta mbalimbali. Zikiwemo ujenzi, uhandisi, usambazaji wa mafuta, nishati na huduma za miundombinu ya migodi.
Huduma nyingine ni chakula, ulinzi, usafirishaji wa wafanyakazi na vifaa vya kujikinga kazini.
Dkt. Kiruswa alisema Serikali itaendelea kuimarisha ushiriki wa wazawa katika sekta ya madini.
Pia alizitaka taasisi za kifedha na sekta binafsi kuwasaidia wajasiriamali wazawa kupata mitaji na ujuzi wa kushindana kwenye zabuni kubwa zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO, Dkt. Venance Mwase, alisema shirika hilo linaunga mkono matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia mradi wa Rafiki Briquette.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati, alisema sekta ya madini inaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi na kutoa ajira kwa vijana kupitia shughuli mbalimbali za mnyororo wa thamani wa madini.


