Na Mwandishi wetu
Dodoma. Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imeanza ukaguzi wa taasisi, mashirika na biashara zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi nchini ili kubaini kiwango cha uzingatiaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.
Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, amesema ukaguzi huo unalenga kubaini kama wadhibiti na wachakataji wa taarifa binafsi wanazingatia matakwa ya kisheria katika ukusanyaji, uchakataji na uhifadhi wa taarifa za watu.
Amesema miongoni mwa mambo yanayokaguliwa ni iwapo taasisi husika imesajiliwa katika rejesta ya Tume pamoja na kama imeteua Afisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Data Protection Officer - DPO) na kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Tume pia inachunguza namna taarifa binafsi zinavyokusanywa, kuchakatwa na kuhifadhiwa pamoja na taratibu zinazotumika wakati wa kuhamisha taarifa hizo nje ya Tanzania kwa mujibu wa Vifungu vya 31 na 32 vya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.
Aidha, wakaguzi wataangalia hatua zilizowekwa na taasisi kulinda taarifa dhidi ya kupotea, kuharibiwa, kubadilishwa au kuchakatwa bila ruhusa, kama inavyoelekezwa katika Kifungu cha 27(1) cha sheria hiyo.
Dkt. Mkilia amesema ukaguzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya kisheria ya Tume katika kuhakikisha taasisi na biashara zinazoshughulika na taarifa binafsi zinazingatia matakwa ya sheria.
Amesema taasisi, mashirika na biashara zitakazobainika kukiuka sheria zitachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, ikiwemo kutozwa faini pale inapobainika kuwa kosa limefanyika.
Hatua hiyo inakuja wakati matumizi ya mifumo ya kidigitali yakizidi kuongezeka katika huduma za umma, biashara, sekta ya fedha, afya, elimu na maeneo mengine, hali inayofanya kiasi cha taarifa binafsi kinachokusanywa na kuchakatwa kuongezeka.
Tume imeendelea kuhimiza wadhibiti na wachakataji wa taarifa binafsi kuweka mifumo na taratibu zinazolinda faragha na usalama wa taarifa za watu, huku wananchi wakitakiwa kufahamu haki zao kuhusu matumizi ya taarifa zao binafsi.

