Kahama, Shinyanga. Wananchi wa Kata za Ikinda na Bugarama katika Halmashauri ya Msalala, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, wameondokana na kero ya kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Ikinda.
Daraja hilo lenye urefu wa mita 11 limejengwa katika barabara ya Ikinda–Buyange na linatarajiwa kuimarisha usafiri pamoja na kurahisisha shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.
Ujenzi wa daraja hilo umefanywa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia Mradi wa RISE, unaotekelezwa kwa fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia.
Wananchi wamesema kabla ya daraja hilo kujengwa, barabara ilikuwa ikikatika wakati wa msimu wa mvua, hali iliyokuwa ikikwamisha usafiri, biashara na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.
Wamesema hali hiyo pia ilikuwa ikihatarisha usalama wa wananchi na mali zao, lakini kukamilika kwa daraja hilo kumefanya changamoto hiyo kuwa historia.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Kahama, Mhandisi Joseph Mkwizu, amesema mradi huo umegharimu Sh milioni 410.02 na umekamilika kwa asilimia 100, huku ukiwa katika kipindi cha matazamio.
Amesema mradi huo haukuishia kwenye ujenzi wa daraja pekee, bali ulijumuisha ujenzi wa kalavati tatu, uchongaji wa barabara yenye urefu wa kilomita nne, kunyanyua tuta na kuweka changarawe kwa urefu wa kilomita moja pamoja na uwekaji wa alama za barabarani.
Daraja hilo lina urefu wa mita 11 na upana wa mita nane.
Mkwizu amesema kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo na bidhaa za biashara kwenda masokoni, huku wananchi wakipata uhakika wa kusafiri hata wakati wa mvua.
Ujenzi wa mradi huo umefanywa na M/S Mashilanga Construction Company Ltd, chini ya usimamizi wa Mhandisi Mshauri NOR-PLAN Tanzania Ltd.
Akifungua rasmi daraja hilo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwangonda, amewataka wananchi kulitunza na kulinda miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu.
Amesema wananchi wanapaswa kuepuka kufanya shughuli zinazoweza kuhatarisha uimara wa daraja na miundombinu yake.
"Utunzaji wa miundombinu ni jukumu la wananchi na Serikali kwa pamoja. Kulinda daraja hili kutasaidia lidumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi," amesema.
Mwangonda pia ameipongeza TARURA kwa usimamizi wa mradi huo na kuhakikisha daraja limejengwa kwa kuzingatia viwango vinavyohitajika.
Kukamilika kwa Daraja la Ikinda ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha mtandao wa barabara na kuondoa vikwazo vya usafiri vinavyoathiri shughuli za kijamii na kiuchumi katika maeneo ya vijijini.

