Bilioni 2 zatumika kuwekeza katika mtambo wa kisasa

Dodoma

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza kutumia teknolojia ya kisasa kufanya uchunguzi wa kina wa udongo kabla ya ujenzi wa barabara, madaraja na miundombinu mingine, hatua inayolenga kuongeza usalama, ubora na uimara wa miradi hiyo.

Teknolojia hiyo inawawezesha wataalamu kupata taarifa kuhusu tabaka za udongo na miamba zilizopo chini ya ardhi, hivyo kusaidia kubaini aina ya msingi na mbinu sahihi za ujenzi kulingana na mazingira ya eneo husika.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa ziara ya waandishi wa habari katika maabara za TARURA, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Tafiti na Udhibiti wa Ubora, Mhandisi Vincent Lwanda, amesema uchunguzi wa udongo ni hatua muhimu katika kuhakikisha miundombinu inayojengwa inakuwa salama, imara na yenye kudumu kwa muda mrefu.

Amesema TARURA imewekeza zaidi ya Sh bilioni 2 katika mtambo maalumu wa kuchimba ardhi na kuchukua sampuli za udongo na miamba kutoka kina kirefu kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu.

“Maabara hizi hazitumiki kwa ajili ya barabara pekee, tunawakaribisha wananchi wanaofanya ujenzi waweze kuleta malighafi zao kwa ajili ya kupima ubora,” amesema.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Vifaa wa Kitengo cha Tafiti na Udhibiti wa Ubora TARURA Makao Makuu, Emmanuel Kilasi, amesema mtambo huo mpya aina ya drilling rig una uwezo wa kuchukua sampuli za udongo kutoka kina cha mita 200 hadi 300, ambazo hutumika kubaini uwezo wa udongo kubeba mzigo na kusaidia kupanga misingi ya barabara, madaraja na majengo.

Amesema TARURA ina maabara kuu jijini Dodoma pamoja na maabara nyingine 16 katika maeneo mbalimbali nchini zinazotoa huduma kwa wananchi, taasisi, wakandarasi na watu binafsi, huku wakandarasi wanaotekeleza miradi ya TARURA wakitakiwa kutumia maabara hizo katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Aidha, amesema matokeo ya vipimo vya maabara hutumika kama sehemu muhimu ya kuthibitisha ubora wa kazi kabla ya malipo, huku matumizi ya teknolojia hiyo yakisaidia kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa ujenzi au baada ya miradi kukamilika.

Ameongeza kuwa maabara hizo pia zimekuwa na mchango katika kukuza ujuzi wa kizazi kijacho cha wahandisi kwa kutoa fursa kwa wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali nchini kupata mafunzo kwa vitendo.

Naye mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Vivian Mwakabaja, amesema mafunzo aliyoyapata katika maabara za TARURA yamemsaidia kuunganisha maarifa ya darasani na utekelezaji halisi wa kazi za uhandisi, ikiwemo kupima ubora wa udongo na kubaini uwezo wake wa kubeba mizigo.