PSSSF na TBN wajenga ushirikiano wa kimkakati kupanua elimu ya hifadhi ya jamii


DAR ES SALAAM

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) wamekubaliana kujenga ushirikiano wa kimkakati kwa lengo la kupanua wigo wa elimu kwa umma kuhusu hifadhi ya jamii, mifumo ya pensheni na uwekezaji unaofanywa na mfuko huo.

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa ziara ya maofisa wa PSSSF katika Makao Makuu ya TBN, Kijitonyama, Dar es Salaam, ambapo pande hizo zilijadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa habari, uelimishaji wa umma na usambazaji wa taarifa sahihi kupitia majukwaa ya kidijitali.

Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema mtandao huo wenye wanachama zaidi ya 200 nchini na Diaspora, uko tayari kutumia uwezo na wigo wa majukwaa ya wanachama wake kuifikia jamii kwa elimu sahihi kuhusu huduma na shughuli za PSSSF.

Hata hivyo, Msimbe alisisitiza umuhimu wa wanachama wa TBN kupatiwa mafunzo kuhusu shughuli, huduma na uendeshaji wa PSSSF ili waweze kutoa elimu kwa umma kwa usahihi na ufanisi zaidi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Msafara wa PSSSF, Abdul Njaidi, alisema ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za mfuko kujenga uhusiano na wadau wa habari na kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii. Aliahidi kuwa hoja na mapendekezo yaliyowasilishwa na TBN yatafanyiwa kazi.

Njaidi alisema PSSSF inalenga kuhakikisha wananchi wanaelewa kwa usahihi masuala ya pensheni, hifadhi ya jamii na uwekezaji unaofanywa na mfuko kwa manufaa ya wanachama na Taifa kwa ujumla.

Naye Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, alisema mtandao huo una historia katika maendeleo ya habari za kidijitali nchini na uko tayari kushirikiana na PSSSF kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inawafikia wananchi kwa lugha nyepesi, sahihi na inayoeleweka.

Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, alisema mtandao huo utatumia waandishi na majukwaa ya wanachama wake kusambaza taarifa sahihi zitakazowawezesha wananchi kuelewa haki, wajibu na fursa zinazopatikana kupitia mifumo ya hifadhi ya jamii.

Ujumbe wa PSSSF uliongozwa na Abdul Njaidi na kujumuisha Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo, huku TBN ukiwakilishwa na Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, mtaalamu wa mawasiliano Cathbert Kajuna na Mdhamini Issa Michuzi.