Darasa la 7 kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kesho Septemba 9, watahiniwa milioni 1.16

Dar es Salaam. 

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza kuwa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) kwa mwaka 2026 utafanyika Septemba 9 na 10, ukihusisha watahiniwa 1,168,649 kutoka shule 20,019 nchini.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Prof. Said A. Mohamed, amesema kati ya watahiniwa hao, wavulana ni 531,467 sawa na asilimia 45, huku wasichana wakiwa 637,182 sawa na asilimia 55. Watahiniwa 1,081,204 watafanya mtihani kwa Kiswahili na 87,445 kwa Kiingereza.

Amesema watahiniwa 4,867 wenye mahitaji maalumu wamesajiliwa, wakiwemo wasioona 82, wenye uoni hafifu 1,591, wenye uziwi 999, ulemavu wa akili 576 na ulemavu wa viungo 1,619.

Ameeleza kuwa masomo yatakayotahiniwa ni Kiswahili, English Language, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi, pamoja na Uraia na Maadili. Mtihani huo utakuwa wa mwisho kutumia mtaala wa sasa.

Prof. Mohamed amesema maandalizi yote yamekamilika, yakiwemo usambazaji wa karatasi za mitihani, mafunzo kwa wasimamizi na kuweka mikakati ya kuhakikisha usalama wa vituo.

Amewataka watahiniwa kuepuka udanganyifu na wasimamizi kuzingatia kanuni za mitihani. Pia ameitaka jamii kutoa ushirikiano ili mtihani ufanyike kwa amani na utulivu.

Kwa watahiniwa wenye mahitaji maalumu, NECTA imeweka utaratibu wa kutumia maandishi ya nukta nundu, maandishi yaliyokuzwa na muda wa ziada kulingana na mahitaji yao

NECTA imewataka wananchi kutoa taarifa za vitendo vya udanganyifu kupitia namba 0759 360 000 au barua pepe esnecta@necta.go.tz.

Mtihani huo utafanyika Jumatano, Septemba 9, na Alhamisi, Septemba 10, 2026.