BOT yawataka wasanii kutumia ushawishi wao kuelimisha utunzaji wa fedha

DAR ES SALAAM: 

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewasihi wasanii na washereheshaji nchini kutumia ushawishi wao kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza na kutumia kwa usahihi noti na sarafu.

Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Tafiti na Uchumi wa BoT, Dkt. Suleiman Misango, wakati akifungua semina iliyowakutanisha wasanii na washereheshaji mbalimbali nchini.

Dkt. Misango amesema utunzaji mzuri wa fedha unasaidia noti na sarafu kudumu katika mzunguko na kupunguza gharama za kuzibadilisha mara kwa mara.

Amesema noti zilizochakaa au kuharibika zinaweza pia kuathiri utendaji wa baadhi ya mashine za ATM na kuongeza gharama za uendeshaji na matengenezo kwa taasisi za fedha.

“Fedha, noti na sarafu usipozitunza vizuri, hata kwenye mashine hasa za ATM hazitoki vizuri. Hivyo, unaongeza gharama kwa mtoa huduma wa fedha, yaani benki,” amesema.

Aidha, BoT imewaelimisha wasanii hao kuhusu shughuli za kifedha zinazohitaji leseni, pamoja na madhara ya kukusanya amana na kutoa mikopo bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania.